Diwani wa Kata ya Masoko, Mbeya Vijijini kupitia Chadema, Edward Mwampamba , juzi alikiweka njiapanda chama chake baada ya kujitoa katika kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri na kumsifia mgombea wa CCM kwamba anafaa kupewa kura zote.
Tukio lilitokea kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo na kuwafanya madiwai wa CCM kushangilia.
Awali Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Anderson
Kabenga alisema kungefanyika uchaguzi wa makamu mwenyekiti na kwamba
wagombea ni Mwampamba wa Chadema na Mwalingo Chisemba ambaye alikuwa
makamu mwenyekiti na pia diwani wa Inyala.
Kibenga alitoa nafasi ya kwanza kwa Mwampamba
kujieleza huku mpinzani wake akiwa nje na ndipo alipowashtua madiwani na
baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa alipotamka kwamba mgombea wa CCM
ni mzuri na anafaa kuendeea kushika wadhifa huo.
“Chisemba alikuwa makamu mwenyekiti na amefanya
kazi vizuri na ni mchapakazi asiye na upendeleo, hivyo mimi nitampa kura
yeye na nawaomba madiwani wote mpigie kura Chisemba,’’ alisema.
Hata hivyo kura zilipigwa kwa kuwapigia wote na
ndipo mgombea wa CCM aliibuka kidedea kwa kupata kura 24 kati ya 25
wakati Mwampamba aliambulia kura 0 huku kura moja ikiharibika.
Akizungumza kwa waandishi wa habari sababu za
kujitoa ghafla alisema aliamua kufanya hivyo kutokana mipango mibaya ya
chama chake katika kuteua mgombea.
‘Mimi nilipigiwa simu na Katibu wa Chadema wilaya,
James Mpalaza kwamba nigombee nafasi hiyo wakati nilikuwa sijajiandaa.
Madiwani wa Chadema tupo watatu hapa wala hatujashirikishwa kwenye kikao
chochote cha uteuzi, hivyo nimejitoa kwa sababu sikujiandaa’’ alisema.
Mwenyekiti wa chama cha APPT –Maendeleo Mkoa wa
Mbeya Godfrey Mwandulusya na Katibu wa NCCR-Mageuzi walioshuhudia tukio
hilo walilaani na kufafanua kwamba lilividhalilisha vyama vya upinzani
nchini. Mwandulusya alisema hatua ya Mwampamba ni dalili kwamba
atajiondoa Chadema kwenye uchaguzi ujao kwa lengo la kuibomoa Chadema.