Na Casiana Ndimbo
Wakulima wa Korosho wa kata ya Masasi Wilayani Ludewa wameiomba serikali kuboresha soko la zao lao ambalo linawaingizia kipato katika kaya zao.
Wakiongea na gazeti hili wakulima hao wamesema kuwa pamoja na wananchi wengi wa kata hiyo kujishughulisha na kilimo cha korosho kama zao la biashara lakini wanakosa soko maalumu ambalo litaweza kununua zao lao kwa uhakika badala ya kuwauzia walanguzi kwa bei ya hasara.
“ Tumechoka kudhulumumiwa na walanguzi, soko la uhakika hatuna hali hii inatukatisha tamaa sisi wakulima kwani tunafanya kazi bila kuona matunda ya kazi zetu, tunaomba serikali itusaidie kupata soko ambalo sisi wakulima tutaweza kuuza zao letu kwa uhakika” alisema Mathia Haule Mkazi wa Masasi.
Wakulima hao wamesema kuwa wanunuzi wa zao lao mara nyingi wananunua kwa vipimo ambavyo sio halali ambayo inazidi kuwakandamiza wakulima na kukosa hali ya kuendelea na kilimo hicho ambacho sasa wengi wanaacha kulima.
“Wanunuzi wanaonunua korosho kwa asilimia kubwa wanawaibia wakulima , wanatumia kipimo ambacho kina ujazo wa kilo nne maarufu kama (kisado) kwa shilingi 1800 tu, ina maana kwa kila kilo moja ni shilingi 450 tu hali ambayo inakatisha tamaa kabisa ya kuendelea kuzalisha zao hili”alisema Stephano Haule.
Kwa mujibu wa Mtendaji wa Kata hiyo Alanus Mbunda amesema kuwa jumla ya kaya 156 wanajishghulisha na kilimo cha korosho lakini idadi hiyo inazidi kupungua baada ya kuona kuwa zao hilo kwa sasa halina faida tena kwao.
Kutokana na taarifa kutoka Bodi ya Korosho Tanzania bei ya korosho kwa m waka 2011/2012 ilikuwa, daraja la kwanzani shilingi 1200 kwa kilo na daraja la pili ni shilingi 960 kwa kilo moja.